Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Yohana
Bahati (1), aliyetekwa juzi katika Kijiji cha Ilelema, wilayani Chato
mkoani Geita na kuokotwa katika Hifadhi ya Biharamulo akiwa amekufa bila
mikono wala miguu, atazikwa leo saa 5 asubuhi katika Kijiji cha Ibondo,
mkoani Geita chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Yohana alitekwa nyumbani kwao saa mbili
usiku, akiwa amebebwa na mama yake. Tukio la kutekwa mtoto huyo
lilifanywa na watu wawili, ambao pia walimjeruhi mama huyo kwa kumkata
mapanga kichwani.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph
Konyo alisema juzi kuwa mwili wa mtoto huyo ulikutwa kwenye shamba la
mahindi katika Kijiji cha Kimasa.
Alisema mwili huo uliokotwa juzi Februari 17, saa 12 jioni kwenye makazi yasiyo rasmi.
Ndugu wa marehemu, walisema kuwa
Kamanda Konyo ameahidi kutoa ulinzi mkali wakati wa mazishi hayo
kutokana na mazingira ya tukio lenyewe.
Katika hatua nyingine, hali ya mama wa
mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, ambaye alitekwa na kufariki dunia baada
ya kukatwa viungo, imeelezwa kuanza kuimarika na kwamba kwa sasa ameanza
kuzungumza polepole pamoja na kula.
Mama huyo, Esther Jonas (30), ambaye
alifanyiwa upasuaji wa kichwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, hali
yake imeanza kuimarika baada ya kuanza kupumua vizuri tofauti na
alivyokuwa jana na kwamba bado madaktari wanaendelea kumpa matibabu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi
jana, Mkuu wa Kitengo cha Dharura BMC, Dk Derick David alisema hali ya
mama huyo kwa sasa imeanza kuwa nzuri tofauti na jana.
0 comments:
Post a Comment