Polisi mkoani Dodoma wanamsaka mkazi wa Chang’ombe Juu, Tisi Malya kwa kumuua askari polisi kwa kumcharanga mapanga wakati akijaribu kumuokoa mtoto wa miezi minane aliyekuwa anataka kuuawa na mtu huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime amemtaja askari aliyeuawa majira ya saa 5:00 asubuhi kuwa ni Joseph Swai.
Akisimulia
mkasa huo kwa waandishi wa habari, Kamanda Misime alisema kuwa askari
huyo aliitikia mwito uliofika kwake wa kuwepo kwa dalili ya tendo la
jinai nyumbani kwa mkazi mmoja wa Chang’ombe Juu katika Manispaa ya
Dodoma.
Alisema
askari huyo alipigiwa simu na Mtendaji wa Mtaa wa Chang'ombe Juu,
akimjulisha kuwa amepokea taarifa ofisini kwake kutoka kwa Oliver
Baltazar(52) mkazi wa Chang'ombe Juu kuwa mtoto wake, Tisi Sirili
anaonekana anataka kumuua au ameshamuua mtoto wake wa miezi minane,
Valerian Tisi.
Alisema
baada ya kupokea taarifa hiyo, askari huyo alikwenda ofisini kwa
mtendaji huyo ambapo waliongozana hadi nyumbani kwa mtuhumiwa.
"Alipofika
askari aligonga mlango huku akijitambulisha kuwa yeye ni askari ili
mtuhumiwa atoke nje, alichofanya mtuhumiwa ni kumnyanyua mtoto wake
mdogo wa miezi minane kwa mkono mmoja kichwa chini miguu juu na kutaka
kumkata kwa panga huku akisema, ‘namkata shingo na sitaki kuona mtu’.
"Askari
aliamua kumwokoa mtoto huyo kwa kumrukia mtuhumiwa, lakini kwa bahati
mbaya aliteleza na ndipo mtuhumiwa akamkata kichwani askari wetu," alisema Misime.
Alisema
pamoja na askari huyo kuanguka, mtuhumiwa aliendelea kumkatakata kwa
panga huku mtendaji na kijana waliyekwenda naye eneo la tukio,
wakikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada.
Alisema
mtuhumiwa baada ya kufanya kitendo hicho cha kinyama, alikimbia akiwa
na panga lake huku nguo zake zikiwa zimetapakaa damu.
Aidha,
alisema katika hekaheka hizo, mama wa mtoto baada ya kuona mtoto
amebwagwa na askari ameanguka chini, naye alimkwapua mtoto na kukimbia
naye mahali pasipojulikana. Alisema polisi wanamsaka baba huyo na mama
huyo kwa ajili ya usalama wake.
0 comments:
Post a Comment