Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewaaga rasmi wananchi wa jimbo hilo huku akiwataka wananchi hao kutosononeka kwa uamuzi wake wa kutoendelea kugombea ubunge wa jimbo hilo, bali wamwombee na kumuunga mkono katika kila uamuzi atakaouchukua.
Zitto
aliwaaga wananchi hao kupitia mkutano wa hadhara mjini Kigoma
uliorushwa moja kwa moja na Kituo cha Radio cha Clouds, ambapo alisema,
kipindi cha miaka 10 kinatosha kwa yeye kuwa mbunge wa jimbo hilo hivyo
kwa sasa ni vyema kijiti akapewa mtu mwingine, ili yeye aweze kusonga
mbele katika kuwatumikia Watanzania kwa nafasi kubwa zaidi.
Hii ni Hotuba Yake Aliyoitoa March 15, 2015
Mwanamapinduzi
na Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas Sankara alisema kuwa ili
kuleta mabadiliko ya kimapinduzi ni lazima kuwa na hali fulani ya
uendawazimu.
Ila
tusiufikirie uendawazimu huu wa kuokota makopo bali ule ukichaa mzuri
wa kuamini katika mambo au misingi fulani na kuisimamia kwa dhati pamoja
na changamoto nyingi.
Kwa
kuamini kwa dhati katika mabadiliko haya na kutaka kuboresha maisha ya
wanakigoma, mwaka 2005 nilikuja kwenu kuwaomba ridhaa ya kuwatumikia
kama mwakilishi wenu Dodoma. Nikiwa na umri wa miaka 29 tu.
Labda
ulikuwa ni msukumo wa matumaini yangu makubwa yanayoambatana na ujana
yaliyowashawishi, kwani mliniamini na kunipa kazi hiyo ya heshima kubwa
ya kuwawakilisha.
Mwaka
2010 mliniamini tena, naamini kutokana na utekelezaji wangu mzuri wa
kazi na mafanikio tuliyoyaweza kuyapata katika jimbo letu.
Hivyo
kwa miaka kumi tumekuwa bega kwa bega katika safari hii ya pamoja ya
kujenga na kuiendeleza jimbo letu, na leo nimekuja kuwashukuru kwa fursa
mliyonipa kwani safari yetu inafikia mwisho. Fursa mliyonipa ni ya
kipekee kwani ilikuwa fursa si tu ya kuwatumikia ninyi bali kulitumikia
Taifa langu.
Katika
miaka kumi hii kuna mambo makubwa tumeyafanya pamoja na kufanikiwa; na
kuna mambo ambayo hatukuweza kuyafanya. Kwa yale ambayo hatukuweza
kuyafanya naomba radhi. Kwa yale ambayo tumeweza kuyafanya naomba
kuwapongeza sana kwa kufanikisha. Kwani kama Mwalimu Nyerere
alivyotuambia kuhusu Uhuru na Maendeleo:
“Uongozi
ni kuongea na kujadili na wananchi, kuwaelewesha na kuwashawishi.
Uongozi ni kufanya kazi pamoja na wananchi na kuonyesha kwa vitendo
mnachotaka kufikia. Uongozi ni kuwa mmoja wa wananchi na kutambua kuwa
mko sawa…. Wananchi hawawezi kuendelezwa bali wanajiendeleza.” Na ndivyo
tulivyofanya kwa miaka kumi, na kwa ushirikiano wenu tumeweza
kufanikisha miradi mikubwa katika Jimbo letu.
Mwaka
2005 tulikuwa hatuna barabara ya lami hata moja. Leo hii, ninapoongea
nanyi tuna barabara za lami zenye zaidi ya kilomita 100 kuunganisha
Jimbo letu na majimbo mengine kwa pande zote za nchi kavu. Vilevile tuna
mradi mkubwa wa kuunganisha vijiji vya ufukweni mwa Ziwa Tanganyika kwa
barabara.
Kiujumla
kwa mkoa wa Kigoma tumefanikiwa kumaliza daraja la Malagarasi na hivyo
kuunganisha mkoa wetu na mkoa wa Tabora kwa lami jambo ambalo lilikuwa
kilio chetu cha muda mrefu sana tokea enzi na enzi. Muhimu zaidi ni kuwa
barabara hizi zinatumika na wananchi, wafanyabiashara na wakulima ili
kuwasiliana, kufanya biashara na kupanua masoko.
Tumefanikiwa
kuongeza huduma ya Nishati ya Umeme kwa kuunganisha vijiji zaidi ya 16
hivi sasa. Changamoto kubwa iliyobakia mkoani kwetu ni uzalishaji mdogo
wa umeme na wenye gharama kubwa sana. Suluhisho la kudumu ni kufanikisha
mradi wa Malagarasi wenye uwezo wa kuzalisha 44MW ambao utakuwa nafuu
na kuwezesha pia kusambaza umeme mikoa jirani ya Katavi na Tabora, na
hata kuuza nchi jirani ya Burundi.
Viongozi
wa kisiasa wa mkoa wa Kigoma watakaoingia kwenye uongozi baada ya
uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka 2015 hawana budi kuweka kipaumbele
kikubwa kwa mradi huu. Bila ya umeme wa uhakika na nafuu hatuwezi kupiga
hatua ya kuongeza thamani ya mazao yetu kwa kujenga viwanda vya
usindikaji na kuongeza ajira ya vijana wetu.
Tumefanikiwa
kuanza miradi ya Bandari na Soko kubwa kijiji cha Kagunga. Lengo likiwa
ni kukuza biashara ya bidhaa kati yetu na nchi ya Burundi. Kigoma ni
mji wa biashara kiasili na biashara ilichukua nafasi kubwa ya uchumi wa
mkoa huu kwa miaka mingi sana. Kuimarishwa kwa miundombinu ya Biashara
ni sehemu ya miradi ya kimkakati katika kuuweka mkoa kuchukua nafasi
yake ya kiuchumi katika nchi yetu.
Katika
muktadha huo ndio maana tunaendelea na miradi ya Bandari Kibirizi na
Bandari ya Nchi Kavu Katosho. Ndio maana tunaendelea na mradi wa Kituo
cha Usafirishaji Mwandiga ( Mwandiga International Transportation
Terminal ) na eneo maalumu la kiuchumi Ujiji. Haya yote tuliyaanzisha
kwa pamoja nanyi ili kuhakikisha kuwa uchumi wetu unazalisha ajira kwa
watu.
Tumefanikiwa
kuongeza udahili wa wanafunzi wa sekondari kwa kuwa na shule katika
kata na baadhi ya kata tumejenga shule kila kijiji. Hata hivyo, tuna
changamoto kubwa sana ya ubora wa elimu katika mkoa wetu. Katika jimbo
la Kigoma Kaskazini zaidi ya 90% ya watahiniwa wa Kidato cha Nne
wanapata madaraja ya mawili ya chini, wakati ule daraja la nne na daraja
la sifuri.
Tumeanzisha
mradi wa majaribio ya kutoa motisha kwa Walimu ili kuona namna bora
zaidi ya kuhakikisha elimu inaboreshwa. Shirika la Twaweza linaendesha
mradi mkubwa wa motisha kwa walimu na baada ya mwaka huu tutakuwa
tumejifunza njia bora za kuongeza ubora wa elimu kwa watoto wetu. Bila
Elimu bora miradi yote niliyoeleza hapo awali haina maana yeyote.
Serikali
imetoa Sera mpya ya Elimu, ni wajibu wetu kuona namna ya kuitekeleza
katika ngazi yetu ili kupata mafanikio. Hata hivyo, uongozi wa kisiasa
utakaoingia baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu hauna budi kujielekeza vya
kutosha katika elimu ya ufundi ili kujenga stadi za kazi kwa vijana
waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Tumefanikiwa
kupanua huduma ya Afya kwa kuboresha Zahanati zetu chache zilizokuwepo
na kujenga zahanati kadhaa mpya na miradi ya vituo vya afya vya Mahembe
na Nyarubanda.
Hata
hivyo nasisitiza sana umuhimu wa kinga kuliko tiba kwani gharama za
afya zimekuwa kubwa sana. Ndiyo maana tulipojadili hili suala,
ilionekana kuwa suluhisho linatakiwa lipatikane kwa kufanya kile ambacho
hatujawahi kufanya ili kuleta maendeleo ya kweli.
Na mniruhusu hapa kunukuu wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alipotuasi kuwa “Maendeleo
ni maendeleo ya watu. Barabara, Majengo, kuongezeka kwa uzalishaji wa
mazao na masuala mengi kama haya si maendeleo, bali ni vitendea kazi tu
vya maendeleo”
Ndiyo
maana kulikuwa na umuhimu wa kutafuta njia mpya na mbadala kuboresha
maisha ya mwananchi, hususan kwa upande wa afya. Uthibitisho wa ubunifu
wetu ni kuwa katika kipindi hiki cha miaka 10 tumefanikiwa kuanzisha
hifadhi ya jamii kwa wakulima.
Tulianza
na Ushirika wa Wakulima wa Kahawa wa RUMAKU ambapo wananchi walijiunga
na NSSF na hivyo kupata mikopo ya muda mfupi, huduma za afya bure na
kujiwekea akiba kwa ajili ya mafao ya muda mrefu.
Mafanikio
makubwa yaliyopatikana yamewezesha wazo hili kusambaa nchi nzima na
hivi sasa wakulima wa Korosho, Chai, Pamba, Tumbaku wanafuata nyayo za
Wakulima wa Ushirika wa RUMAKU.
Hapa
Kigoma wazo hili sasa linatekelezwa kwa wavuvi wa mwambao mwa Ziwa
Tanganyika. Ndoto yetu ni wananchi zaidi ya theluthi moja kwenye nguvu
kazi wawe na Hifadhi ya Jamii.
Natoa
wito kwa wananchi wengine wenye uwezo wa kuchangia hifadhi ya jamii
wajiunge na vikundi vya ushirika na kuchangia ili kufaidika na mafao ya
muda mrefu kama pensheni lakini pia yale ya muda mfupi kama bima ya
afya, mikopo kupitia SACCOS na mengine yatakayoanzishwa kama bima ya
mazao.
Tumefanikiwa
kujenga heshima ya watu wa Kigoma hapa nchini. Hivi sasa watu wa Kigoma
tunatembea kifua mbele bila woga kuliko hapo awali. Kujiamini na
kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa Jamhuri ya Muungano ni wajibu wetu
kama raia. Changamoto za kujiona raia wa daraja la pili zimeondoka na
zinaendelea kutokomezwa.
Juhudi
zetu ni silaha kubwa katika kuhakikisha tunakuwa sehemu ya Jamhuri yetu
katika kila Nyanja za maisha yetu. Nafurahi kupata fursa ya kushiriki
nanyi katika kujenga heshima hiyo ya Mkoa wetu. Nitaendelea kushiriki
katika kudumisha heshima hiyo.
Nimejifunza
mengi sana katika safari hii ya utumishi kwenu. Kama nilivyosema hapo
awali, mliamua kufanya kile kisichozoeleka katika siasa ya nchi yetu kwa
kunipa jukumu hili nikiwa kijana mdogo.
Naamini
kuwa ule ukichaa wangu mzuri wa kusimamia misingi ya kuleta maendeleo
kwa wananchi wangu na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia
nimezipigania. Na katika safari hii nimejenga marafiki wengi sana na
pengine hata maadui ingawa hao ni wachache. Lakini haijalishi kwani mi
binafsi sina uhasama na binadamu mwenzangu.
Katika
utumishi wangu kwenu, bungeni nimejifunza namna nchi yetu inaendeshwa.
Katika kujifunza huko kuna mambo kadhaa nimefanya ya kujivunia na
mengine ni makosa. Mliniruhusu kufanya makosa na kuyarekebisha makosa
hayo kwa hiyo kukomaa zaidi.
Shukrani
za dhati ziwaendee wazee wangu ambao mliniongoza mpaka hapa tulipofika
na kunishauri hata kunionya pale palipohitajika. Kwa ujumla nimejifunza
kuwa mzalendo zaidi kwa nchi yangu na kuwatumikia watu wa nchi hii.
Ndio
maana hamkunisikia tu kutetea watu wa Kigoma pekee, bali watu maeneo
mengine ya nchi yetu na makundi mbalimbali ya kijamii kama Wakulima,
Wafanyakazi, Wasanii, Wavuvi, Wana michezo na wana habari.
Katika
safari hii ya miaka 10 kuna watu nimewafurahisha na kuna watu
nimewaudhi. Kwa wale niliowaudhi ninaomba radhi. Kwa wale
niliowafurahisha ninaomba wasiache kuniongoza na kunishauri kila wakati.
Haikuwa
safari rahisi na sikutegemea iwe rahisi. Kiuhalisia ilikuwa safari
ngumu yenye mafunzo makubwa kwangu. Ilikuwa ni safari yangu kama
kiongozi na pia safari yangu binafsi ya kupevuka kifikra na kupata
mafunzo kuhusu maisha.
Ukifika
ulikokuwa unakwenda katika safari, unaweza kutathmini mengi kuhusu
safari hiyo, lakini mwisho wa siku unatakiwa ujue kama safari hii
ilikuwa njema ama la. Ninajivunia safari hii na ninasema kwa dhati
kabisa ilikuwa ni safari njema.
Ni
wakati sasa wa kutoa nafasi kwa nguvu mpya kuongoza Jimbo letu. Kushika
kijiti pale ninapoishia. Kurekebisha pale nilipokosea. Kuimarisha pale
nilipofikia.
Sitakuwa
mbunge wenu baada ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba lakini nitaendelea
kutetea maslahi ya Mkoa wa Kigoma na Taifa letu kwa njia nyingine.
Sitaacha
ule uendawazimu mzuri aliyoizungumzia Thomas Sankara unaoleta maendeleo
ya kimapinduzi. Na misingi ni ileile na maadui ni walewale ambao
mwasisi wetu Mwalimu Nyerere aliyokuwa anasema tupambane nao, yaani
umaskini, ujinga, maradhi na sasa tumeongeza ufisadi.
Kizazi
chetu kina jukumu la kipekee kuendeleza mapambano haya na nitaendelea
kuhakikisha tunafanya mapinduzi na kuwa na Taifa lenye misingi madhubuti
ya uwajibikaji ili kuondoa kila aina ya ufisadi na kutumia rasilimali
za nchi kuondoa umasikini, ujinga na maradhi.
Asanteni sana Kigoma Kaskazini!
0 comments:
Post a Comment