Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia) akitoa ufafanuzi kuhusu utafiti wa wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) unaofanywa na chuo hicho kwa kushirikiana na Shirika la Wafanyabiashara kutoka nchini Finland (FBMA) kwa lengo la kubaini fursa za biashara zilizopo , faida, changamoto na mchango wao katika maendeleo ya taifa pindi watakapoingizwa kwenye mfumo rasmi unaotambulika kisheria.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Simon Msanjila (kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu mchango wa utafiti wa shughuli za wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) unaofanywa na chuo hicho kwa kushirikiana na Shirika la Wafanyabiashara kutoka nchini Finland (FBMA) utakavyochangia maendeleo ya sekta ya biashara nchini.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Simon Msanjila (kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu mchango wa utafiti wa shughuli za wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) unaofanywa na chuo hicho kwa kushirikiana na Shirika la Wafanyabiashara kutoka nchini Finland (FBMA) utakavyochangia maendeleo ya sekta ya biashara nchini.
Na Aron Msigwa – MAELEZO
9/4/2015, Dar es Salaam
9/4/2015, Dar es Salaam
Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) kwa kushirikiana na Shirika la Wafanyabiashara kutoka nchini Finland (FBMA) kinafanya utafiti wa wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) kwa lengo la kubaini fursa za biashara zilizopo , faida, changamoto na mchango wao katika maendeleo ya taifa pindi watakapoingizwa kwenye mfumo rasmi unaotambulika kisheria.
Akizungumzia utafiti huo leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema amesema kuwa kwa kipindi kirefu wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kama wamachinga wamekuwa katika malumbano na mamlaka za miji na majiji kote nchini kutokana na kukosa mfumo rasmi unaotambua biashara zao.
Amesema chuo chake kwa kuliona jambo hilo kikishirikiana na Shirika la Wafanyabiashara wa Finland (FBMA) kimeamua kuendesha utafiti huo kuanzia mwaka 2014 na kuongeza kuwa matokeo ya awali yaliyopatikana ndani ya mwaka mmoja yamebainisha kuwa jiji la Dar es salaam lina wamachinga zaidi ya Laki saba (700,000) wanaofanyabiashara zao nje ya mfumo rasmi unaotambulika kisheria.
“Katika utafiti tumegundua kuwa Dar es salaam ina wamachinga wengi zaidi kuliko maeneo mengine walio nje ya mfumo rasmi unaotambuliwa na Serikali hii ni fursa, kwa sasa hakuna mfumo wowote unaotambua uwepo wao na baadhi yao wamekuwa wakilumbana na vyombo vya usalama na mamlaka husika jambo lililojenga uadui miongoni mwao” Amesema Prof. Mjema.
Amesema katika kutatua changamoto hizo utafiti huo utaangalia jinsi gani wamachinga watatambulika kisheria katika mfumo rasmi , pia kukisaidia Chuo cha Elimu ya Biashara kuandaa mitaala na programu mbalimbali za masomo ya biashara kwa vijana hao ambao wengi wao wameishia elimu ya darasa la 7 ili kuwajenge uwezo wa kutunza kumbukumbu za biashara zao pamoja na kuiwezesha Serikali kuweka utaratibu wa wafanyabiashara hao kufikiwa na huduma muhimu katika maeneo yao.
Aidha, amesema utafiti huo utawasaidia wafanyabiashara hao kuepuka hasara wanayoipata mara kwa mara kutokana na bidhaa zao kukamatwa na wakati mwingine kuharibiwa na mamlaka zinazohusika wakati wa oparesheni mbalimbali za kuwaondoa katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kufanya biashara.
“Katika utafiti huu tunapendekeza kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa kuwatambua wamachinga wote kote nchini ili waweze kujulikana na shughuli wanazofanya na mchango wao kwa taifa” Amesisitiza.
Katika hatua nyingine Prof. Emanuel Mjema amesema kuwa chuo chake kiko katika hatua za mwisho za uanzishaji wa mafunzo ya Shahada ya Ualimu katika Biashara ili kuziba pengo la uhaba wa walimu wa kufundisha masomo ya Biashara katika shule za Sekondari na vyuo kote nchini.
Amesema chuo chake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kimefikia uamuzi huo kufuatia utafiti uliofanywa na jopo la wataalamu wa maandalizi ya Mtaala wa kufundishia programu hiyo mwaka 2012 uliobaini uwepo wa kiwango kikubwa cha uhitaji wa waataalam wa kufundisha masomo ya biashara wenye taaluma ya ualimu.
“Sisi kama chuo cha Elimu ya Biashara tumeona uhitaji uliopo nchini wa kukosa wataalam wa kufundisha masomo ya Biashara wenye taaaluma ya ualimu ndio maana tumeamua kuanzisha mtaala huu wa kufundishia wanafunzi wa Shahada ya Elimu katika Biashara ili tupate wahitimu bora watakaofundisha wanafunzi wetu na kukidhi mahitaji ya soko” Amesisitiza.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof.Simon Msanjila akifafanua kuhusu utafiti huo amesema kuwa Serikali itanufaika zaidi kutokana na kutambua mchango wa wafanyabiashara hao pindi itakapowaingiza katika mfumo rasmi.
Amesema wafanyabiashara hao wanapotembeza bidhaa zao barabarani, mitaani pamoja na maeneo mbalimbali ya miji hufanikiwa kusanya zaidi ya shilingi elfu thelathini kwa siku ( 30,000) jambo linalotia matumaini kwa sekta ya biashara na Serikali iwapo watathaminiwa na kujengewa mazingira mazuri ya kutambuliwa
0 comments:
Post a Comment