WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema wiki ijayo atatangaza majina ya wafanyakazi wa Kampuni ya Reli (TRL) watakaofukuzwa kazi, kutokana na kutokuwa na tija kwenye shirika.
Aidha, alisema huduma ya usafiri wa Reli ya Kati, zitaanza mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2015, hivyo kuwataka wananchi wanaoishi kando kando ya reli kuondoka, kwani wanahatarisha maisha yao.
Alisema hayo jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa TRL mkoani hapa wakati wa ziara yake aliyoifanya kutembelea taasisi zilizopo kwenye wizarayake.
“Serikali inawekeza ili tuone tija na kama tija haionekani, basi uongozi wa juu una shida, hatuwekezi pesa na kunyima sekta nyingine halafu Reli ikabaki vile vile, fanyeni kazi kwa ubunifu la, nitafukuza wote,” alisema Waziri Mwakyembe.
Alisema, “Shirika limejaa mtandao wa wezi tu, ukiwemo wa mafuta, nimewaonya iliyopita, kazi yenu wizi tu na kulifanya shirika likose tija. Leo tunaleta vifaa vya mabilioni ya kodi za wananchi, kichwa kimoja cha treni kinagharimu Sh bilioni saba, halafu kinapinduka kwa uzembe uzembe tu”.
Aliwataka wafanyakazi wa TRL kuwa na vipaumbele katika utekelezaji wa majukumu yao, vikiwemo vya kuhakikisha vichwa vya treni havidondoki kwa ajili ya uzembe na kwamba vikidondoka kwa ajili ya uzembe, viongozi watafute kazi nyingine za kufanya, sio ndani ya Shirika hilo.
Alisema hiki ni kipindi cha TRL kutengeneza fedha na hataki kuisikia malalamiko kutoka kwao, kwani vifaa wanavyo, waende kwenye mabenki na kufanya kazi kwa tija ili walipane mishahara mizuri.
“Hili Shirika lazima libadilike ndani ya miezi sita, mkishindwa nendeni mkachome mkaa, nitaajiri wengine wanaoweza kufanya mabadiliko kwenye shirika, hatuwezi kufanya kazi kimzahamzaha tu, tunaondoa fedha katika maeneo muhimu mengine na kupeleka kwenye reli halafu tija haionekani, haikubaliki hata kidogo,” alisema.
Alisema katika kipindi kifupi, baada ya serikali kununua hisa zote za TRL, imenunua mabehewa 270 na imetoa fedha nyingine kwa ajili ya kununu mabehewa 210 na vichwa 13 vya treni vimekwishalipiwa na kuagizwa.
Alisema jitihada hizo za serikali, zimeihamasisha Benki ya Dunia kununua mabehewa 44 na vichwa vitatu huku Mamlaka ya Bandari ikitoa Sh bilioni 17 kwa ajili ya kuunda vichwa vitano vya treni.
Alisema TRL ilianzishwa ili iweze kujitegemea, lakini imeshindwa kujitegemea na Serikali inaendelea kulipa watumishi mishahara.
0 comments:
Post a Comment