C/HQ/ADM/PRESS/37 21/12/2014
Ndugu waandishi wa habari,
Tumewaita
hapa baada ya kupata fununu kuwa Rais Jakaya Kikwete anataka
kutumia hotuba yake ya kesho( leo ) na wanaoitwa, “Wazee wa Dar es Salaam”
kutetea wizi mkubwa wa fedha za umma uliofanyika ndani ya Benki Kuu
(BoT), kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow.
Tunazo taarifa kuwa Rais
Kikwete amejipanga kuuhadaa umma kwa kisingizio cha uchunguzi wa Ikulu,
ili kuwalinda watuhumiwa ambao wanapaswa kuwajibishwa kwa kuwafuta
kazi, kushitakiwa na kufirisiwa. Habari tulizozipata kutoka ndani ya
Ikulu kwenyewe, zinasema Rais Kikwete amejiandaa kumlinda Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara
hiyo, Eliakim Maswi.
Tunapenda kumtahadharisha Rais Kikwete
kuachana mara moja na mpango wowote wa kumlinda Profesa Muhongo na
Maswi, ambao hadi muda huu walipaswa siyo kuwa nje ya ofisi, bali
walitakiwa kuwako gerezani.
Ndugu waandishi wa habari;
Ndugu waandishi wa habari;
Umma
unafahamu kwamba anayejiita mmiliki wa kampuni ya PAP, alikabidhiwa
fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow, kabla ya kuwa mmiliki halali
wa kampuni hiyo.
Ushahidi wa hili, unapatikana katika kesi
iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na James Rugamalira, dhidi ya
Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndulu, kampuni ya PAP na Benki ya
Stanbic, tawi la Tanzania.
Rugamalira alifungua shauri hili
baada ya kukuta fedha zilizokuwapo kwenye akaunti ya Escrow
zimeshachukuliwa, wakati yeye akiwa bado hajamaliziwa kiasi chake cha
fedha alichokuwa anadai baada ya kuuza asilimia 30 ya hisa zake katika
IPTL.
Katika shauri hilo lililomalizika kwa njia ya usuluhishi wa
mahakama, Mahakama Kuu ya Tanzania, pamoja na mengine, ilisema
yafuatayo:
- Kwamba baada ya kampuni ya VIP kulipwa fedha zake zilizotajwa katika mkataba, itailipa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kodi yote ya mapato inayotokana na mkataba inayofikia Sh. 38, 186,584,322/- (bilioni thelathini na nane milioni mia moja na themani na sita laki tano na elfu themanini na nne na mia tatu ishirini na mbili) kama zilivyokadiriwa na TRA kupitia Kadirio la Kodi Na. 427038820 la tarehe 15 Januari 2014. Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani tarehe 8 Januari 2014 na VIP ENGINEERING AND MARKETING LIMITED (VIP) kama mdai na iliunganisha kesi za madai Na. 49/ 2002 na kesi ndogo Na. 254 YA 2003.
- Kwamba baada ya VIP kulipa kodi hiyo kwa TRA, fedha zake zilizobaki hazitalipwa kwake mpaka pale itakapowasilisha Cheti cha Kulipa Kodi na hati za kuhamisha asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL kwa mwanasheria wa PAP, na wasilisho hilo lilitakiwa kufanyika kabla ya saa 10 jioni ya tarehe 27 Januari 2014.
- Aidha, baada ya kulipwa kiwango chote cha mkataba kilichotajwa hapo juu, VIP itathibitisha uridhiaji na ukubali wake wa kuhamishwa asilimia 70 ya hisa za MECHMAR CORPORATION (MALAYSIA) BERHAD katika IPTL, na uridhiaji na ukubali huo unarudishwa nyuma kuanzia tarehe ya mauzo na uhamishaji wa hisa hizo kwa PAP.
Ndugu waandishi wa habari;
Hii maana yake nini? Jibu
ni kwamba, wakati PAP analipwa kiasi cha Sh. 321 bilioni kutoka BoT,
haikuwa mmiliki halali wa IPTL. Hakuwahi kusajili hisa zake BRELA wala
hakuwa amenunua asimia 30 ya hisa za VIP.
Huu ni wizi ambao
hauwezi kuvumiliwa na umma na chama chetu, ambacho ni tegemeo la
Watanzania katika kulinda rasimaliza za taifa, ikiwamo fedha na kutetea
haki za wanyonge na kusimamia misingi ya uwajibijkaji, hakiwezi
kunyamaza na kumuacha Rais Kikwete akitekeleza mradi wake wa kulinda
wezi. Hakiwezi!
Kwa msingi huo, tunamtaka Rais Kikwete katika
hotuba yake ya kesho( leo), kuwajibisha wale wote walioshiriki kwa namna moja
au nyingine, katika kutekeleza wizi huo.
Miongoni mwao, ni Prof.
Muhongo, Maswi, Gavana wa BoT, Prof. Ndulu, Katibu Mkuu
wizara ya Fedha, Silviacius Likwelile, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredric Werema na Mkurugenzi Mkuu wa
Tanesco, Felicesmi Mramba.
Ndugu waandishi wa habari,
Watanzania
bado wanakumbuka kauli iliyotolewa bungeni wakati wa mkutano uliopita
kuwa familia ya Rais Kikwete nayo iko nyuma ya sakata hili ikiwa
mnufaikaji mkubwa kupitia kwa mtu aitwaye Albert Marwa ambaye ana
uhusiano na familia hiyo.
Kitendo cha Rais Kikwete kushindwa
kuchukua hatua madhubuti katika jambo hili, utakuwa ni ushahidi wa wazi
kuwa kigugumizi ambacho kimekuwa kikiikabili serikali yake katika jambo
hili kinasukumwa na jambo kubwa nyuma yake, ikiwamo kujilinda binafsi na
kulinda familia yake.
Ndugu waandishi wa habari,
Suala
la miamala iliyofanyika kupitia Benki ya Stanbic katika sehemu ya
kashfa hiyo ya Akaunti ya Escrow, si suala la kufanyia mzaha au kupuuzwa
hata kidogo katika ufisadi huu.
Ni kupitia benki hiyo ndiko
kiwango kikubwa cha fedha zaidi ya Sh. 160 bilioni, zilibebwa kwa
magunia, malumbesa na sandarusi ndani ya siku moja mchana kweupe, tena
tunaambiwa wengine walikwenda kwa magari yenye nambari za serikali na
fedha hizo zilipelekwa Ikulu ambako Rais Kikwete anafanyia kazi na
kuishi.
Ni ukweli ulio wazi kuwa hakuna benki ndani ya nchi yetu
inayoweza kufanya miamala ya mabilioni ya fedha kwa kiwango hicho, bila
BoT kuidhinisha. Kwa mantiki hiyo hiyo, Gavana Prof. Ndulu hawezi
kukwepa uwajibikaji kwenye jambo hili zito kwa kuwa alilifahamu na
kulilidhia.
Tunatarajia Rais Kikwete ataueleza umma wa Watanzania
hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi hawa wa umma na siyo kuja na
visingizio vya miamala iliyochukuliwa katika Benki ya Mkombozi.
Watanzania
wanasubiri kusikia Rais Kikwete anachukua hatua dhidi ya Waziri wa
Fedha Saada Mkuya Salum ambaye wakati fedha katika Akaunti ya Escrow
zinatolewa kati ya Septemba na Desemba mwaka jana, alikuwa ndiye Kaimu
Waziri wa Fedha.
Wakati huo, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk.
William Mgimwa alikuwa katika matibabu ya ugonjwa uliopelekea kifo chake
ambacho kimedaiwa kuwa na utata, nchini Afrika Kusini.
Ndugu waandishi wa habari;
Aidha,
katika kuwatafuta watu waliochukua fedha za Akaunti ya Escrow kwa
magunia na malumbesa, Rais Kikwete aweke wazi kile kinachoonekana
ushirika wa ufisadi kati ya serikali, Benki ya Stanbic na chama chake –
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Katibu Mkuu wa chama hicho,
Abdulahman Kinana.
Tunazo taarifa za uhakika kwamba Kinana
alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo na Mjumbe wa Bodi ya Stanbic,
na ambaye alikuwa kiunganishi kikubwa kati ya serikali, CCM na Benki
katika kufanya miamala ya aina hiyo ya kifisadi.
Rais Kikwete
anatarajiwa kumwagiza Kinana awataje watu waliokwenda kuchukua mabilioni
ya fedha kwa malumbesa, magunia na sandarusi, vinginevyo atakuwa
anahalalisha madai haya kuwa ushirikiano huu si bahati mbaya na ndiyo
maana, fedha kutoka Akaunti ya Escrow ya Tegeta, zilipitia katika benki
hiyo.
………………………
Arcado Ntagazwa
MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI
CHADEMA.
CHADEMA.
0 comments:
Post a Comment