Bush kuiongoza Marekani kama Rais kwa mara nyingine. | HABARI MATUKIO TEKNOLOJIA NDANI NA NJE YA Tz

Bush kuiongoza Marekani kama Rais kwa mara nyingine.


Gavana wa zamani wa Jimbo la Florida nchini Marekani Jeb Bush ametangaza kujiuzulu nafasi mbalimbali ambazo anashika kwenye makampuni kadhaa pamoja na nyadhifa anazoshika kwenye bodi za  taasisi  mbalimbali zisizo za kibiashara ikiwa ni ishara ya dhamira ya gavana huyo wa zamani ya kuingia moja kwa moja kwenye mbio za kuwania urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2016 .

Kwa mujibu wa msaidizi wa karibu wa mwanasiasa huyo , Jeb ambaye ni mdogo wa rais wa zamani wa Marekani George Walker Bush ataangalia uhusiano alio nao kwenye biashara tofauti katika kipindi cha mwaka  huu akiwa na lengo la kujiondoa kwenye biashara na kuingia kikamilifu kwenye siasa akiwania nafasi ya kukiwakilisha chama cha Republican kwenye uchaguzi wa mwakani .

Jeb Bush alitangaza mwishoni mwa mwaka 2014 kuwa anafuatilia kwa karibu mchakato wa urais japo hajaweka wazi azma yake ya kuingia kwenye mbio hizo .
Jeb Bush anatarajiwa kutangaza azma ya kuwania urais wa Marekani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.

Msemaji wa Bush Kristy Campbell ameithibitisha hatua hii akisema kuwa ilikuwa kiasi cha muda kwa haya kutokea kwani ni ukweli usiofichika kuwa Jeb amekuwa na kiu ya kuingia ikulu na hatua yake ya kujiondoa taratibu kwenye biashara imetazamwa kama hatua ya mwanzo ya kusafisha njia ya kutimiza azma yake .

Msemaji wa Jeb pia amethibitisha kuwa Jeb ataendelea kubaki kwenye bodi za makampuni ambayo yeye ni mshirika ikiwemo kampuni yake ya ushauri wa masuala ya biashara ya Jeb Bush and Associates .

Tayari Bush alishajiuzulu kwenye bodi ya wakurugenzi kwenye kampuni za Rayonier Inc , Tenet Healthcare  Corporation na benki ya Uingereza ya Barclays .
Rais wa zamani wa Marekani Mzee George Herbert Walker Bush (kushoto) na rais mwingine wa zamani wa Marekani George Walker Bush (katikati) na Jeb Bush (kulia) katika picha ya pamoja .

Endapo Bush ataingia kwenye mbio za kuwania urais na kufanikiwa kuingia ikulu atakuwa mtu wa tatu kwneye ukoo wa Bush baada ya Baba yake Mzazi George Herbet Walker Bush Sr na kaka yake mkubwa George Walker Bush ambaye alikuwa rais wa Marekani katika miaka ya 2000 mpaka 2008 .

SHARE

Unknown

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment