Kiongozi wa Kanisa la Waadventista
Wasabato (SDA) duniani, Askofu Ted Wilson anatarajiwa kuwasili nchini
leo kwa ziara ya kikanisa ya siku nne.
Taarifa
iliyotolewa na kanisa hilo, jijini Dar es Salaam, inaonesha kuwa
kiongozi huyo anakuja nchini kushiriki Sherehe za Utume zilizoandaliwa
na kanisa hilo na kujumuisha nchi zingine 11 za Afrika Mashariki na
Kati.
Pamoja
na kushiriki kwenye sherehe hizo, lakini kiongozi huyo atashiriki
kwenye kuzindua miradi mbalimbali ya afya na elimu ya kanisa hilo
nchini.
Sherehe
hizo ambazo zinatarajiwa kuvuta zaidi ya watu 50,000 kutoka nchi hizo
11 na sehemu zingine duniani, zitakwenda sambamba na utoaji wa huduma
mbalimbali za kijamii, ikiwa ni pamoja kupima afya kwa magonjwa
mbalimbali kama ya moyo, sukari, Ukimwi na magonjwa mengine.
Juzi
Kiongozi wa Mawasiliano wa kanisa hilo katika ukanda wa Kati na
Mashariki mwa Afrika, Mchungaji Steven Bina alisema mkutano huo wa siku
nne, ambao unafanyika Uwanja wa Taifa ni wa aina yake na wa kwanza
kufanyika nchini.
Katika
mfululizo wa sherehe hizo, jana kulizinduliwa ujenzi wa Makao Makuu ya
Jimbo la Kusini Mashariki mwa Tanzania (SEC), ambayo yatajengwa katika
maeneo ya Kwembe, nje kidogo ya Dar es Salaam.
Shughuli
zingine ambazo zilifanyika juzi ni uzinduzi wa kituo cha vitabu,
ambacho kipo eneo la Ilala na kitatoa huduma kwa wakazi wa Dar es
Salaam, ambao watahitaji vitabu mbalimbali vikiwemo vya afya na aina vya
vyakula vinavyofaa kwa mwili wa binadamu. Kituo hicho kilizinduliwa na
Mkurugenzi wa Idara ya Uchapishaji ya kanisa hilo duniani, Mchungaji
Howard Faigao.
Miongoni
mwa shughuli zingine ambazo zitafanywa na kanisa leo ni utoaji wa
vitabu 1,000 na jozi 300 za viatu kwa ajili ya shule za msingi, na
utoaji wa vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari. Vitu hivyo
vitatolewa kwa manispaa ya Ilala, ambayo ndio itakayovisambaza mahali
ambako kuna mahitaji.
Mkutano
huo unahusisha washiriki kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Rwanda,
Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Eritrea,
Somali, Ethiopia, Sudan Kusini na Djibout. Baadhi ya kwaya pia zitatoka
nje ya Bara la Afrika.
Tamasha
hilo kubwa la kitume, linatarajiwa kuhutubiwa kesho na Rais Jakaya
Kikwete. Lakini pia kutakuwepo na viongozi wengine wapatao 400 wa kanisa
hilo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Sherehe
hizo zenye kauli mbiu ya “Kusherehekea Mibaraka ya Mungu katika
Utume”, zinafanywa na kanisa hilo ikiwa ni njia ya kujivunia mafanikio
makubwa yaliyofikiwa katika upelekaji wa injili na utoaji wa huduma za
jamii.
0 comments:
Post a Comment