Ofisi ya Bunge imesema haijapata barua yoyote kuhusu kuvuliwa uanachama kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).
Kauli
ya hiyo ya Bunge imekuja siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kutangaza kumvua uanachama Zitto, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Bunge, Dk.
Thomas Kashililah, alisema kutokana na hali hiyo, Zitto bado ni mbunge
halali wa Kigoma Kaskazini na kwamba anapaswa kuendelea na shughuli zake
kwa mujibu wa sheria.
Dk
Thomas Kashililah, amebainisha kuwa endapo Bunge litapata taarifa rasmi
ya Chadema kumvua uanachama Zitto, lazima Bunge hilo lifanye kwanza
uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili ndipo litoe uamuzi.
Pia
amesema sakata la mbunge wa Bunge hilo kuvuliwa uanachama na chama
chake si la kwanza, kwani tayari kuna mbunge aliyevuliwa uanachama na
chama chake lakini Bunge hilo halikumvua uanachama wake baada ya
kumaliza uchunguzi wake. Hata hivyo hakumtaja mbunge huyo.
“Utaratibu
ulivyo, chama huliandikia Bunge kuhusu kumvua uanachama mbunge na Bunge
kabla ya uamuzi wowote hufuatilia kwanza sababu za kuvuliwa uanachama
huo, ili kujiridhisha kama zilikuwa halali au la,”alisema Kashililah.
Alisema
baada ya hapo Bunge hilo huwasiliana na Msajili wa Vyama vya Siasa ili
ofisi hiyo ya msajili iweze kupitia Katiba ya chama husika na kupitia
sababu za chama husika zinazoweza kumvua uanachama mwanachama wake na
kama kweli zimekiukwa.
“Baada
ya suala hilo kupelekwa kwa msajili wa vyama vya siasa, Spika wa Bunge,
hutoa uamuzi baada ya kuchunguza na uamuzi huo, hupelekwa kwa Tume ya
Uchaguzi ya Taifa (NEC) kwa ajili ya kufanyiwa kazi zaidi,” alisisitiza.
Aidha alisisitiza: “Si
lazima Spika akubaliane na uamuzi wa kutengua ubunge wa mbunge husika
kwani kama haikuwa halali kwa mbunge huyo kuvuliwa uanachama, Spika
hubatilisha uamuzi wake wa kumvua ubunge mhusika,” alisema.
Alisema
Spika Anne Makinda katika kipindi chake alishawahi kutoa uamuzi wa
kubatilisha mbunge fulani kuvuliwa ubunge hata baada ya chama chake
kumvua uanachama.
Akizungumzia
suala hilo, Zitto, alisema kwa upande wake bado ni mbunge na anaendelea
na kazi yake ya Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali
(PAC) hadi pale atakapopatiwa taarifa rasmi ya kuvuliwa uanachama na
ubunge wake.
“Naendelea
na kazi kama vile hakuna kilichotokea, sina taarifa yoyote ya kuvuliwa
uanachama wangu wala ubunge, habari hizi nimezisikia kwenye vyombo vya
habari, sijaitwa na Mahakama kuambiwa kinachoendelea,” alisema Zitto.
Alisema
kwa sasa anaendelea kuongoza kamati hiyo na jana alikutana na
menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), leo kamati yake
inatarajia kukutana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pia watakutana na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mwanasheria Mkuu kuhusu mapato ya
akaunti za madini.
Aidha
alisema pamoja na kuendelea kama kawaida na shughuli zake za kibunge
bungeni, pia anatarajia kesho kwenda Kigoma kwa ajili ya shughuli za
maendeleo jimboni kwake, kabla ya kuhudhuria vikao vya Bunge
vinavyotarajiwa kuanza rasmi Machi 17, mwaka huu.
Alisema
kwa upande wake, anachukulia suala hilo kama changamoto ambayo inazidi
kumkuza na kumkomaza katika medani za siasa nchini na duniani kote.
Kwa
upande wake, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema chama
hicho kinajitahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa kuzingatia sheria na
taratibu zote, ikiwemo kuandaa na kuiwasilisha wakati wowote barua
inayomvua uanachama Zitto, ili suala hilo lifanyiwe uamuzi mapema.
“Kwa
sasa suala hili la Zitto limewaingia Watanzania wengi, sasa sisi
tunataka tulifanyie kazi mapema, ili uamuzi ufanywe mapema na suala hili
liishe. Kuna mambo mengi ya maana yanahitaji kujadiliwa kitaifa kama
vile masuala ya uandikishaji katika Daftari la Wapiga kura kwa mfumo wa
BVR,”alisema.
Mwanasheria
Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye juzi alitangaza kuwa chama hicho
kimemvua uanachama mbunge huyo, jana alimwambia mwandishi kuwa, jopo la
wanasheria wa chama hicho litaifikisha taarifa ya Zitto kuvuliwa
uanachama kwa Kamati Kuu ya chama ifikapo Mei, mwaka huu.
Alisema, "Kutokana
na utaratibu uliopangwa wa Kamati Kuu kukutana kila baada ya miezi
mitatu, suala la Zitto litasubiri kikao kingine cha kawaida cha kamati
hiyo kitakachokaa mwezi Mei. Kikao kilichopita kilikaa Februari mwaka
huu".
0 comments:
Post a Comment