Polisi Achomwa Mkuki Ubavuni | HABARI MATUKIO TEKNOLOJIA NDANI NA NJE YA Tz

Polisi Achomwa Mkuki Ubavuni



POLISI wa kituo cha Kinesi wilayani Rorya mkoani Mara, Konstebo Deogratius amejeruhiwa kwa kuchomwa mkuki ubavuni.

 

Alichomwa mkuki wakati akiwa na wenzake walipokuwa wakipambana kujaribu kuwaondoa zaidi ya watu 2,000 waliovamia mgodi wa dhahabu wa kampuni ya Acacia wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime.

 
Askari huyo mwenye namba G 7606 amelazwa katika Hospitali ya Shirati akitibiwa jeraha hilo.
 
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa alisema kuwa kutokana na uvamizi huo, polisi inawashikilia watu sita wanaotuhumiwa kuingia ndani ya mgodi na kujeruhi baadhi ya askari akiwamo huyo aliyechomwa mkuki kwa lengo la kuiba mawe ya dhahabu.
 
Kamanda huyo alibainisha kuwa watu hao zaidi ya 2,000 waliingia ndani ya mgodi huo, saa 7:00 mchana wakiwa na silaha za jadi kama vile mapanga, mishale, mikuki na marungu.
 
“Waliingia ndani ya mgodi na kuanza kufanya vurugu kwa kuwashambulia askari na walinzi waliokuwa wakilinda mgodi huo kwa nia ya kutaka kupora mawe ya dhahabu,” alisema na kuongeza:
 
 “Askari wetu wa Jeshi la Polisi wakishirikiana na walinzi wa mgodi huo waliwazuia wavamizi hao kwa kurusha mabomu ili wasiingie kupora mali.
 
“Walijitahidi kupambana na kundi hilo la wavamizi hao na kufanikiwa kuwaondoa ndani ya mgodi huo, lakini askari wetu PC Deogratius aliyekuwa katika operesheni hiyo alijeruhiwa na mkuki ubavuni”.
 
Alisema alikimbizwa kupatiwa matibabu ya awali katika Hospitali ya Wilaya Tarime na kwa sasa amehamishiwa kupata vipimo vya x-ray katika Hospitali ya Shirati wilayani Rorya ambapo anaendelea na matibabu.
 
Alisema watu sita wanaoshikiliwa na polisi wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma za kuvamia na kuingia ndani ya mgodi bila idhini wakiwa na lengo la kufanya uhalifu na kujeruhi askari.
SHARE

Unknown

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment