Madawa ya kulevya
Siku
za wasafirishaji na wauzaji wa dawa za kulevya kwenda China sasa
zinahesabika baada ya Jeshi la Polisi na kitengo chake cha Dawa za
Kulevya kubaini majina ya vigogo wanaofanya shughuli hiyo na kusema
imeanza kuwashughulikia kimyakimya.
Majina
ya vigogo hao yametajwa na Watanzania waliofungwa katika magereza
mbalimbali nchini China kupitia barua zinazoeleza namna matajiri wa hapa
nchini wanavyowatumia vijana kusafirisha dawa za kulevya.
Wafungwa
hao ambao wengi wanatumikia kifungo cha maisha na wengine kati ya miaka
20 hadi 25 wanalalamika kuwa matajiri wanaowatuma hawachukuliwi hatua
za kisheria, licha ya wao kuwataja kwa majina na kuweka wazi ushahidi
kwa viongozi wa Serikali wanaowatembelea magerezani, China.
Hata
hivyo, Kamishna wa Kikosi cha kupambana na Dawa za Kulevya nchini,
Godfrey Nzowa pamoja na kuthibitisha kupata taarifa hizo, alisema baadhi
ya wafanyabiashara wanaodaiwa kuwa vigogo wa unga wameshakamatwa.
Kaimu
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Diwani Athumani
alisema Jeshi la Polisi linafuatilia ushahidi wa barua hizo na tayari
limeshafanyia kazi baadhi.
“Tunafuatilia
na tayari tumeshafanikiwa kwa upande mmoja ila hatuwezi kuweka wazi
kila kitu kwa sababu kama ujuavyo suala la dawa za kulevya ni nyeti mno
na pengine tunaweza kuharibu ushahidi,” alisema Athumani.
Barua
zilizotumwa na wafungwa hao ambazo tumeziona, zilitumwa kupitia kasisi
anayetoa huduma kwa wafungwa magerezani, Hong Kong na China, John
Wotherspoon wa Parokia ya Notre Dame, Shing Tak Street, Kowloon, China
ambazo zinawataja baadhi ya wafanyabiashara papa wa dawa za kulevya
ambao majina yao tunayahifadhi kwa sasa.
Taarifa
zaidi kutoka kwa Mchungaji Wotherspoon, zinaeleza kuwa hivi sasa wapo
Watanzania zaidi ya 200 katika magereza hayo na 130 kati yao,
wameshahukumiwa vifungo mbalimbali na wengine wapo rumande.
“Kati
ya Mei na Juni 2013, zaidi ya Watanzania 50 walikamatwa Hong Kong na
China. Ukiwasikiliza wanalia na wanataka kuwasiliana na ndugu zao hata
kwa barua,” inasema sehemu ya barua pepe ya Mchungaji Wotherspoon
aliyoituma kwa gazeti hili.
Oktoba
18, 2013 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa ziarani China aliambiwa
kuwa kulikuwa na vijana 175 ambao walikuwa wamefungwa katika magereza ya
nchi hiyo baada ya kukamatwa na dawa za kulevya na kwamba baadhi yao
walikuwa wakikabiliwa na adhabu ya kifo.
Barua
ya mmoja wa wafungwa, Michael Mmasi Daudi anayetumikia kifungo cha
miaka 23 katika Gereza la Stanley, ilimtaja mfanyabiashara mkubwa wa Dar
es Salaam ambaye anamiliki maduka ya simu kuwa ni gwiji wa kuwatumia
vijana wadogo kubeba dawa hizo.
Wotherspoon
alisema anatarajia kuzungumza na viongozi na wanausalama wa Tanzania
kuhusu namna ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya.
Alisema
kati ya Aprili Mosi hadi Juni 16 mwaka huu, Watanzania 16 walikamatwa
katika Uwanja wa Ndege wa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya.
Barua
Katika
barua hizo wafungwa walisema wamekuwa wakitishwa na wafanyabiashara wa
dawa za kulevya iwapo watathubutu kuwataja kwa vyombo vya dola.
Mfungwa
Suedi Maulidi ilisema alikamatwa na kilo moja ya dawa za kulevya katika
Jimbo la Macau na kumtaja tajiri anayemtuma kuwa ni mkazi wa Magomeni
ambaye anamiliki mabasi na biashara nyingine.
Alisema
tajiri huyo amekuwa akiwatumia vijana wasio na ajira kusafirisha dawa
za kulevya maeneo ya Magomeni na kuwatisha kuwa endapo watamtaja
atawaua.
Wafungwa
wengine walimtaja Mtanzania anayeishi Guangzhou kwamba amekuwa akitumia
mgongo wa biashara ya vipuri vya magari na simu kuficha biashara haramu
inayoifanya.
Uchunguzi
umebaini kuwa mfanyabiashara huyo anatajwa kuwa na ofisi katika Mtaa wa
Dongfeng, Hong Kong na anashindwa kurudi nchini kukwepa mkono wa
sheria.
Habari
zinasema kuwa licha ya kusakwa na polisi, pia ndugu wa wafungwa
wanamtafuta mfanyabiashara huyo ili kumkabidhi mbele ya vyombo vya
sheria. Nzowa alisema mkono wa Serikali unajua taarifa zake na
kilichobaki na kumfikia tu.
Mfungwa
mwingine, Ambrose Mahimbo anayetumikia kifungo cha miaka 24, alieleza
jinsi maofisa wa uhamiaji wa China wanavyowanyanyasa Watanzania
wanaokwenda nchini humo kwa shughuli mbalimbali.
Mahimbo
alisema maofisa hao wanapoona hati ya kusafiria ya Mtanzania, moja kwa
moja humpeleka katika chumba cha mahojiano na upimaji wa kina kwa kuwa
inafahamika wengi wao hubeba ‘unga’.
Mahimbo anasema baadhi yao huvuliwa nguo na wengine huwekwa uwanja wa ndege kwa zaidi ya saa nane wakifanyiwa ukaguzi.
Pamoja
na kuwataja wafanyabiashara hao, barua nyingi za wafungwa hao ziliwaasa
vijana wa Kitanzania kuacha biashara hiyo huku zikieleza mateso
wanayoyapata katika magereza hayo ikiwamo kazi za suluba na chakula
kibaya.
0 comments:
Post a Comment