KAMA KWELI UNAMPENDA UNAKUBALIJE KUMUACHA KIRAHISI? | HABARI MATUKIO TEKNOLOJIA NDANI NA NJE YA Tz

KAMA KWELI UNAMPENDA UNAKUBALIJE KUMUACHA KIRAHISI?

Ninachotaka kukizungumzia leo ni kuhusu watu kuachana katika mazingira ambayo wengi wasingetarajia. Zipo ndoa ambazo zimefungwa kwa mbwembwe sana lakini hazikudumu na ukiuliza utaambiwa chanzo ni mambo madogomadogo tena ya kuvumilika.
Yapo ambayo kiukweli hayavumiliki kabisa. Kuna sababu ambazo ukitajiwa kuwa ndizo zilizosababisha  flani na flani kuachana, utasema hata ingekuwa wewe usingeweza kuvumilia lakini kuna nyingine ukitajiwa utashangaa na hutaweza kuamini.
Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu unayempenda huwezi kukubali kuachana naye kirahisi.  Yapo mambo ya kuumiza na kukera ambayo mtu anaweza kukufanyia lakini kutokana na unavyompenda unavumilia na kuyaacha yapite.
Hicho ndicho kinachotakiwa kufanyika. Tufahamu kwamba mapenzi ni kitu cha kuwa nacho makini sana. Yapo mengi yatatokea, yapo mengi utaambiwa kuhusu mpenzi wako lakini kikubwa ni wewe kupima kisha kutokuwa na papara ya kumuacha.
Iko hivi, ukisikia wawili waliotokea kupendana mpaka wakafikia hatua ya kuoana wameachana kwa sababu ya kufumaniana, hutashangaa sana.
Na hii ni kutokana na ukweli kwamba usaliti ni sababu ya msingi inayosababisha wengi kuachana. Mimi naweza kuvumilia na kutomuacha mke wangu baada ya kumfumania lakini uamuzi huo unaweza kuwashangaza wengi ambao huenda ingewatokea wao wangechukua uamuzi wa kuwaacha wapenzi wao.
Lakini ifahamike kuwa watu tunatofautiana, huenda mimi nina moyo tofauti wa kuchukulia mambo makubwa kuwa madogo.
Sitakiwi kuonekana mjinga kwa kufanya uamuzi huo kwani huenda inatokana na namna nilivyopenda na ninavyoweza kuchukulia usaliti huo kama njia ya kuboresha uhusiano wangu. Lakini pia wewe unaweza kumuacha mpenzi wako kwa kumfumania na wengi wakaona umefanya uamuzi sahihi kwa kuwa wanajua madhara ya kusalitiwa na namna inavyouma.
Kwa maana hiyo sasa, mpenzi wako akikusaliti na ukamuacha hilo haliwezi kuwa suala la kuwashangaza sana watu lakini kile ninachokizungumzia mimi ni watu kuachana kwa mambo ya kijinga. Mtu anapelekewa maneno ya uongo kwamba mume wake kaonekana maeneo f’lani na mwanamke, mke badala ya kuchunguza anakuwa mkali.
Anaamsha timbwili na wakati mwingine kuomba hata talaka. Mtu wa sampuli hii utaamini kuwa sababu hiyo ndiyo iliyofanya aombe talaka kweli?
Achilia mbali hao, wapo ambao waliachana kwa sababu eti mwanaume anahisi anasalitiwa. Eti kwa sababu huwa anamuona mke wake anawasiliana sana na mtu flani basi anahisi anaibiwa na bila kuchunguza anakuwa mkali, kutokuelewana kunatokea na mwisho kuachana.
Jamani, hisia tu zikufanye uamue kumuacha mwenza wako uliyeapa kudumu naye? Una uhakika gani na kile unachokifikiria? Watu wakidhani umepata kimwana mwingine ndiyo maana unatafuta sababu ya kumuacha huyo uliye naye watakosea?
Ifike wakati tuheshimu mahusiano yetu. Kama kweli umeamua kuingia kwenye ndoa na mtu uliyetokea kumpenda basi kamwe usikubali kuachana naye kirahisi. Yapo ambayo yakitokea na ukaamua kumuacha watu hawatakuona ni mtu wa ajabu kwa sababu kibinadamu kila mmoja ataona una hoja lakini hili la kuachana kirahisi linaashiria aidha hukuwa na mapenzi ya kweli au umemchoka tu.
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba, wanaopendana kwa dhati watavumiliana sana na pale itakapotokea wameachana basi ujue Mungu ndiye ameona iwe hivyo. Kama uko kwenye uhusiano jaribu sana kuulinda kwa gharama zozote. Ziba masikio yako ili wambeya wasikupenyezee maneno ya kukuharibia lakini pia mvumilie mwenza wako katika yale ambayo yanavumilika.
Kumuacha siyo suluhu. Unaweza kumuacha huyu ambaye umemfumania lakini huwezi kujua huyo mwingine utakayempata itakuwaje.
Wapo waliowahi kuwafumania wapenzi wao wakawasamehe na leo hii wanaishi maisha mazuri. Kwa nini? Kwa sababu waliamini usaliti unaweza kuboresha uhusiano wao na ikawa hivyo.
Mimi nikutie moyo wewe ambaye umekuwa ukiumizwa sana na mpenzi wako ambaye unampenda. Najua mara kadhaa unajiwa na mawazo ya kutaka kuachana naye lakini wakati mwingine jaribu kuwa mvumilivu, ukiona maji yamekufika shingoni na unakoelekea ni hatari zaidi, hapo sasa ukiamua kujitoa wala hutakuwa umekosea
SHARE

Unknown

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment