Akizungumzia
hali ya usalama nchini jana katika hotuba yake ya mwisho wa Februari,
Rais Kikwete pia amekuja juu kuhusu mauaji kwa watu wenye albinism na
kusema vitendo hivyo vinafedhehesha, kudhalilisha taifa na havivumiliki.
“Kwa
jumla hali ya usalama ni nzuri, hata hivyo kuna matukio ya kiusalama
ambayo ningependa kuyazungumzia. La kwanza ni mashambulizi yenye sifa
za ujambazi na mwelekeo wa kigaidi. Na, la pili ni la mauaji ya watu
wenye ulemavu wa ngozi,” alisema Kikwete.
Akizungumzia
mauaji ya albino yaliyoanza kuibuka tena mwaka jana na mwaka huu, baada
ya hali kuwa tulivu mwaka 2011, Rais Kikwete amekubali kukutana na
viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi, kwa
lengo la kuwasikiliza na kuangalia jinsi ya kumaliza mauaji ya watu hao,
yanayofanywa kwa imani ya ushirikina.
“Naungana
na Chama cha Albino Tanzania kulaani ukatili huu na kutaka watu wote
wanaojihusisha na ukatili huu wasakwe, wakamatwe, wafikishwe mahakamani
na kupewa adhabu kali inayowastahili wanapopatikana na hatia,” alisema Rais Kikwete.
“Nimekubali
wiki ijayo kukutana na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha
Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi, kuwasikiliza maoni yao na kuangalia jinsi
ya kumaliza tatizo hili. Kwa kweli, mauaji ya albino ni jambo
linalofedhehesha na kudhalilisha taifa letu, ni vitendo
visivyovumilika…hatuna budi sote kushikamana na kuhakikisha tunapambana
nao kisawasawa na kuwashinda, tusikubali kamwe waturudishe kule kubaya
tulikokuwa zamani, "alisisitiza Rais Kikwete.
Rais Kikwete aliongeza “Nimesikitika
na mauaji ya ndugu zetu albino. Ni vitendo vya kinyama ambavyo
havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yeyote. Naamini
ushirikiano wa karibu kati ya serikali na jamii utatuwezesha kutokomeza
mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na kuliondolea taifa letu
aibu hii”.
Alisisitiza,
watu wenye ulemavu wa ngozi ni wanadamu kama walivyo wasio na ulemavu
huo na wana haki sawa ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao, kama
walivyo wanadamu wengine.
Alitaka
jamii kushikamana kuhakikisha mapambano dhidi ya wahalifu hao
yanafanywa na kuwakamata, wafikishwe kwenye vyombo vya sheria, haki
itendeke.
“Niwahakikishie
ndugu zangu albino wakati wote serikali inalipa uzito mkubwa suala la
kudhibiti na kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ,
watuhumiwa kadhaa wa mauaji hayo wako waliokwishahukumiwa na wengine
bado wanaendelea kusakwa,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza
serikali itatumia mbinu na maarifa iliyotumia kukabili wimbi kubwa la
mauaji hayo miaka ya nyuma. Aliomba wananchi kutoa ushirikiano wa
kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya mauaji na kukata viungo vya watu
wenye ulemavu wa ngozi.
“Kutokomeza
kabisa matukio ya mauaji na ukataji wa viungo vya watu wenye ulemavu wa
ngozi ni jambo linalowezekana, kikubwa ni watu kuacha imani za
ushirikina, eti kiungo cha albino kinaweza kukusaidia, ni imani potofu
kabisa, uvuvi, uchimbaji madini, biashara ni vichocheo vya uovu huu,” alisema Rais Kikwete.
Aliomba wananchi kusaidia kutoa taarifa kuhusu wanunuzi wa viungo hivyo na waganga wanaochochea mahitaji ya viungo vya albino.
Tukio
la kwanza liliripotiwa mkoani Geita tangu Aprili 17 mwaka 2006.
Watuhumiwa wa mauaji hayo waliuawa na wananchi wenye hasira. Mwaka 2007
kulikuwa na matukio saba na mwaka 2008 matukio ya mauaji ya albino
yaliongezeka kutokana na watu 18 waliouawa.
Kikwete
alisema jitihada za serikali zilifanywa kwa kushirikiana na wananchi na
hivyo mauaji yalipungua na kuwa tisa mwaka 2009. Mwaka 2010 matukio
hayo yalipungua na kuwepo na tukio moja.
Mwaka
2013 mmoja aliuawa na wengine watatu walijeruhiwa. Mwaka 2014 waliuawa
albino watatu na wawili walijeruhiwa. Januari mwaka huu, tukio moja
mkoani Geita limeripotiwa.
Matukio
ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yametokea katika mikoa 10 kati
ya mikoa 30 nchini. Mikoa hiyo ni Mwanza wenye matukio 13, Kagera
(sita), Tabora (matano), Geita (manne) na Mara matukio manne.
Mikoa mingine ni Kigoma (manne), Simiyu (matatu), Shinyanga (mawili), Arusha (moja) na Mbeya tukio moja.
Rais
alisema katika kipindi cha takribani miezi 12, kumekuwa na matukio ya
watu kuvamia vituo vya Polisi, wengine kuchoma moto na kupora silaha.
“Pia kumekuwepo na matukio ya kuwashambulia Polisi walioko kwenye doria
na wengine kuporwa silaha,” alisema.
Kikwete
ambaye amepongeza polisi wakishirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania kwa kazi kubwa waliyofanya, amesema vyombo vya usalama
vinaendelea kufanya kazi ya uchambuzi wa kila tukio na kulipa nafasi
yake stahiki; kwa maana kama ni la ujambazi au ugaidi.
“Mafanikio
tunayaona, kama nilivyoeleza na kama tulivyosikia kule Tanga hivi
karibuni, ni matunda ya ushirikiano huo. Hata hivyo, nimewataka
waendelee kuwasaka watu hawa waovu popote walipo ili wafikishwe
mahakamani na kuzirejesha mikononi mwa Polisi silaha zote zilizoporwa,” alisema.
Rais
alitaja maeneo ya matukio husika ni Newala, Ikwiriri, Kimanzichana,
Ushirombo, Songea, Pugu Machinjioni na Tanga ambako jumla ya silaha 36
ziliporwa, askari saba walipoteza maisha na wengine kupata majeraha.
Vituo
vya Polisi vilivyovamiwa na silaha kuporwa kwenye mabano ni Newala
mkoani Mtwara (3), Ikwiriri wilayani Rufiji (7), Kimanzichana wilayani
Mkuranga ni silaha tano ambazo kati yake, mbili ni za polisi na tatu za
raia waliokwenda kuzihifadhi.
Uvamizi
ulifanyika pia kwenye vituo vya Ushirombo wilayani Bukombe (18), Pugu
Machinjioni (1), Tanga (2) na Ruvuma ambako kulikuwepo na matukio mawili
ya Polisi kushambuliwa lakini silaha hazikuporwa.
Kwa
mujibu wa Rais Kikwete, silaha 18 zilizoporwa Ushirombo zimepatikana na
watu 10 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo wamekamatwa.
Kuhusu
tukio la Tanga, Kikwete alisema silaha moja kati ya mbili zilizoporwa
imepatikana na watuhumiwa saba wametiwa mbaroni, wanne kati yao ni
waliokuwa wamejificha katika mapango ya Kiomoni wilayani Tanga.
Kwa
upande wa watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la Ikwiriri,
walikamatwa na kwenye tukio la Newala, silaha zote tatu zimepatikana na
watu wawili wametiwa nguvuni.
“Upelelezi
unaendelea wa kuzipata silaha zilizoporwa ambazo hazijapatikana mpaka
sasa kila moja kutoka Kimanzichana, Pugu Machinjioni na Tanga,” alisema.
Aidha,
Kikwete alitoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa karibu na vyombo vya
usalama hususani Jeshi la Polisi kupata mafanikio zaidi dhidi ya
uhalifu kwa kutoa taarifa za kuwapo vitendo viovu au nyendo za watu
waovu wanavyokusudia kufanya wahalifu au taarifa za waliokwishafanya
uhalifu.
Kikwete pia alitaka wananchi kuacha kushabikia watu waovu, wala kueneza taarifa zao potofu kwenye mitandao ya kijamii.
“
Tutumie mitandao ya kijamii kuponda fikra zao potofu, fikra zao hasi na
vitendo vyao viovu pamoja na kuwafichua wao na mambo yao mabaya
wayafanyayo,” alisema.
Pia,
Kikwete aliwapongeza wananchi waliotoa taarifa zilizowezesha kuzuia
uhalifu kufanyika au kufanikisha kuwatia mbaroni wahutumiwa wa vitendo
vya ujambazi na ugaidi.
Wakati
huohuo, Rais Jakaya Kikwete ameagiza Hazina kuhakikisha inaitengea
fedha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kazi ya kuandikisha wapiga
kura kwa Mfumo wa Teknolojia ya Utambuzi wa Alama za Vidole ‘Biometric
Vote Registration’ (BVR) ikamilike kama ilivyopangwa.
Aidha, ametaka watu kuwa na subira kuhusu Kura ya Maoni, wazingatie masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni na Kanuni zake.
Akihutubia
taifa jana, Kikwete alisema Serikali itatimiza ahadi yake kwa kufanya
kila linalowezekana kuwezesha Tume kirasilimali iweze kutimiza jukumu
hilo.
Kauli
ya Rais imekuja siku chache baada ya vyama vinavyounda Ukawa hivi
karibuni kukaririwa katika mkutano na waandishi wa habari, vikisema Nec
inakabiliwa na ukosefu wa fedha, utakaoifanya Tume ishindwe kutekeleza
majukumu yake ya uandikishaji wapiga kura kwa ufanisi.
Ukawa
kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu
Lipumba vilitaka Serikali kuelekeza nguvu na kuiongezea fedha Nec.
Vyama
hivyo vilisema uhaba huo wa fedha umefanya Tume kuwa na upungufu wa
mashine 7,750 na pia kutokuwa na watumishi wa kutosha.
“Nimekwishawakumbusha
Hazina kuhusu umuhimu wa zoezi hili kufanikiwa kama ilivyopangwa.
Nimewataka wahakikishe wanatoa kipaumbele cha kwanza katika mgao wa
fedha. Kama haifanyiki, naomba Tume waniambie mimi mwenyewe,” alisema.
Aidha,
Kikwete alisema changamoto za kiufundi zilizojitokeza na zile
zinazotokana na upya wa mfumo kwa watumiaji, zimefanyiwa kazi na
watengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika awamu hii ya uandikishaji
nchi nzima.
Alisema,
kuanza kutumika kwa teknolojia hii ni kielelezo cha utashi wa Serikali
kuwa nchi iwe na uchaguzi ulio huru, wazi na haki.
Akizungumzia
kuanza kwa uboreshaji wa daftari na uandikishaji wapiga kura ulioanzia
katika mji wa Makambako, Kikwete alisema wananchi wamejitokeza kwa wingi
kuliko ilivyotarajiwa.
Alisema
kati ya Februari 23 hadi 25 mwaka huu, Tume ilitegemea kuandikisha
wapiga kura 9,541 lakini kutokana na mwamko wa wananchi wameweza
kuandikisha wapiga kura 13,042.
Kikwete
alisema kila kituo kilikuwa kinaandikisha kati ya wapiga kura 80 na 150
kwa siku, huku lengo la Tume ni kuandikisha wapiga kura 32,000 katika
Halmashauri ya Makambako ambako kwa siku wanatarajia kuandikisha watu
4,320.
“
Naambiwa kuwa hesabu za juzi na jana wameandikisha hadi wapiga kura
6,000 kwa siku. Kwa kasi hii na kama mambo yatakwenda kama
inavyotarajiwa, lengo litafikiwa na hata kuvukwa.”
Kikwete
aliipongeza Tume kwa hatua waliyofikia katika uandikishaji na kuwa hali
hiyo inaondoa hofu iliyoanza kuingia miongoni mwa baadhi ya watu kuwa
huenda zoezi hili lisingefanikiwa.
Kabla
ya uzinduzi uliofanywa mwezi uliopita na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Tume ilifanya majaribio ya uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia
mashine za BVR katika kata 10 za halmashauri za Kinondoni, Kilombero na
Mlele kazi iliyofanyika kwa mafanikio kwa kuvuka malengo ya
uandikishaji.
Kilombero walifikia asilimia 110.9 ya lengo, Mlele asilimia 101 na Kawe ilikuwa ni asilimia 105.67.
Aidha,
Kikwete ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanakwenda kujiandikisha
kwa mujibu wa ratiba ya uandikishaji katika maeneo yao kama
itakavyotolewa na Tume.
“Msifanye ajizi maana hakutakuwepo na fursa nyingine ya kujiandikisha kabla ya uchaguzi mkuu baada ya fursa hii kupita. "
Kikwete aliongeza,“Naendelea
kusisitiza kuwa watakaojiandikisha wakati huu ndio watakaopiga kura ya
maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na ndio watakaopiga kura katika
uchaguzi mkuu, kwani vitambulisho vya zamani havitatumika."
Kikwete
pia alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa vyama vya siasa, Serikali,
dini na asasi za kiraia kuungana na Serikali na Tume katika
kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi wakajiandikishe.
“Naomba tusiwachanganye wananchi kwa kutoa taarifa zisizokuwa za kweli na kuwafanya wakaacha kujiandikisha.”
Alisema,
Serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila atakayejitokeza
anaandikishwa na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati changamoto
zitakapojitokeza.
“Kupiga
kura kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa au kuchagua Rais, Wabunge na
Madiwani ni haki na wajibu wa kila raia. Kuipata haki hiyo na kuweza
kutimiza wajibu huo kunategemea kuwa na kitambulisho cha mpiga kura.
Bila ya hivyo haiwezekani.”
Akizungumzia
Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, alisema Tume pia itatoa
maelekezo kuhusu kampeni ya Kura ya Maoni wakati ukiwadia.
“Naomba
watu wawe na subira na kuzingatia masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni
na Kanuni zake. Tukifanya hivyo, zoezi hili muhimu na la kihistoria
litatekelezwa kwa usalama na utulivu. Watu watafanya uamuzi kwa uhuru,
uelewa, amani na usalama.”
Kikwete
alisema utekelezaji wa mchakato huo wa kura ya maoni, umeshaanza na
unaendelea ikiwa ni pamoja kuandikisha wapiga kura na usambazaji wa
katiba hiyo.
Alisema hadi mwishoni mwa Februari, vitabu 1,558,805 vilikuwa vimechapishwa na nakala 1,341,300 kusambazwa.
Nakala 1,141,300 zimesambazwa kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara na nakala 200,000 zimegawiwa Zanzibar.
Alisema
kwa upande wa Tanzania Bara kila kata imepewa vitabu 300. Kwa vile
kata zina wastani wa vijiji vitano hii ina maana kwamba kila kijiji
kimepata vitabu 60.
Kikwete
alisema mpaka sasa asasi za kiraia 495 zimejiandikisha kwa ajili ya
kutoa elimu kwa umma, asasi 420 ni za Bara na 75 za Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment