Licha
ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ufafanuzi wa sakata la uchotaji fedha
kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu na kutangaza
kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya viongozi na watendaji, nchi wahisani
wamesema bado suala hilo linawachanganya na wanasubiri tamko la
Serikali.
Nchi
hizo, ambazo zilizuia takriban Sh1 trilioni za ufadhili na kuchangia
nakisi ya bajeti ya Serikali, juzi zilikiri kuanza kuruhusu sehemu ya
fedha hizo baada ya baadhi ya maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano
kuanza kutekelezwa, ikiwa ni pamoja na kumvua uwaziri Anna Tibaijuka,
kumsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi na kumuweka kiporo waziri wake, Sospeter Muhongo na kusababisha
Jaji Fredrick Werema kujivua wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ameshaeleza kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali.
Hata
hivyo, akizungumza juzi, Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini, Timothy
Clarke alisema kwamba Serikali imeonyesha jitihada za mwanzo, lakini
wanasubiri kuona hatua kali zaidi zikichukuliwa pamoja na kuja na kauli
moja kuhusu fedha hizo.
Alisema
alichobaini ni kwamba wananchi wengi wanataka kujua hatima ya sakata
hilo ndiyo maana walitumia vyombo vya habari kufanya mijadala mbalimbali
kuzungumzia wizi wa fedha za escrow ambazo haijawekwa wazi kuwa ni za
umma ama ni za Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.
Balozi
Clarke alisema kwa upande mwingine, Serikali imeonyesha tabia ya kusita
katika kutoa uamuzi kwenye suala hilo na kwamba walitarajia kusikia
tamko kali pamoja na tamko la kuzuia vitendo hivyo visiendelee.
Alieleza
kuwa hadi sasa nchi nyingi hazijaipa fedha Tanzania kama zilivyokuwa
zinatarajiwa kwa kuwa bado zinasubiri hatua zaidi kutoka serikalini.
Sakata
la escrow, lililohusu uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka akaunti hiyo,
lilisababisha Taasisi ya Marekani ya MCC inayosaidia nchi zinazoendelea,
kutangaza kusitisha kusaini mkataba wa awamu ya mpango huo wa maendeleo
kuishinikiza Serikali kushughulikia kashfa hiyo.
Bodi
ya Wakurugenzi ya MCC ilitoa taarifa yake Desemba 16 mwaka jana,
ikieleza kuwa mkutano wake wa Desemba 10 mwaka huu uliruhusu kuanza
maandalizi ya kusaini mkataba wa awamu ya pili ya mpango huo, lakini
ulielezea hofu na masikitiko kuhusu hali ya rushwa inavyoendelea
Tanzania.
Fedha
ambazo Tanzania ilipaswa kupata kupitia mradi huo wa MCC awamu ya pili
ni Dola 450 milioni ambazo ni sawa na Sh765 bilioni.
“Japokuwa
bodi ilipiga kura kwa dhati kabisa ya kuiruhusu Tanzania iendelee na
maandalizi kwa ajili ya mkataba wa pili, inaihimiza Serikali ya Tanzania
kuchukua hatua thabiti na mahsusi za kukabiliana na rushwa kama sharti
la msingi kwa bodi hiyo kufanya uamuzi wa mwisho wa kuidhinisha mkataba
huo.
Sakata
la escrow lilihusisha fedha zilizokuwa zimehifadhiwa Benki Kuu wakati
kesi baina ya Shirika la Umeme (Tanesco) na IPTL zikipambana mahakamani.
Pande hizo mbili zilikubaliana kufungua akaunti hiyo ya escrow ili
kutunza fedha ambazo Tanesco ilitakiwa iilipe IPTL ikiwa ni malipo ya
ununuzi umeme.
Hata
hivyo, akaunti hiyo ilifungwa kwa njia ambayo ilitia shaka na fedha
hizo kulipwa kwa Kampuni ya Pan African Power Solution Limited (PAP)
ambayo ni mmiliki mpya wa IPTL na kukiwa na mambo mengi yaliyotakiwa
kufanyiwa kazi kabla ya malipo hayo, ikiwa ni pamoja na kulipwa kwa kodi
ya Serikali na kukokotoa upya gharama ambazo Tanesco ilitakiwa ilipe
baada ya mzozo wao kuisha mahakamani.
Pia,
fedha hizo zililipwa kwa James Rugemarila aliyekuwa akimiliki asilimia
30 ya hisa za IPTL na ambaye baada ya malipo alitoa mgawo wa fedha kwa
watu kadhaa, wakiwamo viongozi wa dini, watumishi wa umma, mawaziri na
Mwanasheria Mkuu wa zamani, hali iliyotia shaka zaidi kuhusu fedha hizo.
Tayari
Tibaijuka amewajibishwa baada ya kupokea Sh1.6 bilioni kutoka kwa
Rugemarila, hali kadhalika Andrew Chenge, ambaye pia alipewa Sh1.6
bilioni na William Ngeleja (40.4 milioni) wametakiwa kuondolewa kwenye
uenyekiti wa Kamati za Bunge sambamba na Victor Mwambalaswa na Fredrick
Werema, akitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu kwa
maelezo kuwa ushauri wake haukueleweka na kuzua tafrani.
Naye
Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose alisema mazungumzo na
Serikali bado yanaendelea na kwamba hali itaendelea kuwa nzuri kadri
mazungumzo yanavyoendelea.
“Bado tunaendelea na mazungumzo na Serikali huku tukisubiri tamko,” alisema Dianna.
Taarifa
iliyotolewa na Mwenyekiti wa mfuko wa maendeleo wa wahisani, Sinikka
Antila juzi ilieleza kuwa mpaka sasa zimekwishatolewa Dola 84 milioni
sawa na asilimia 15 ya msaada wote kwenye bajeti ya 2014/2015.
Kwa
upande wake, kiongozi wa mabalozi waliopo nchini, Juma Mpango alisema
Tanzania imeonyesha jitihada katika kuleta maendeleo na kupambana na
rushwa.
Balozi
Mpango, ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),
alisema Serikali imeonyesha nia ya kupunguza matukio ya kifisadi.
“Tumefuatilia
namna ambavyo Tanzania imefanya vita kubwa kuondoa madhara ya ufisadi
katika nchi, ilikuwa kubwa sana,” alisema Balozi Mpango.
0 comments:
Post a Comment