Waziri
wa Ujenzi Dk John Magufuli amevitaka vyombo vya dola kuingilia kati
suala la rushwa kwenye vituo vya mizani za kupimia uzito wa magari
yanayosafirisha mizigo, akisema rushwa hiyo imekithiri.
Magufuli
alitoa agizo hilo alipotembelea na kukagua kituo cha mizani cha Mpemba
wilayani Momba, ambapo alipita kituoni hapo kwa kushtukiza, alipokuwa
katika ziara yake ya kukagua barabara akielekea wilayani Ileje.
Kupita
kwa Magufuli kwenye mizani hiyo, kulitokana na yeye kujionea namna
barabara ya kati ya Mbeya na Tunduma ilivyoharibiwa, kutokana na malori
yanayosafirisha mizigo inayozidi uzito unaotakiwa kutoka Bandari ya Dar
es Salaam kwenda mpaka wa Tunduma kabla ya kuvushwa kuelekea nchi
jirani.
Baada
ya kufika kituoni hapo, alihoji maofisa waliokuwa zamu ni kwa nini
barabara ionekane kuharibika upande mmoja wa magari yanayotoka Mbeya
kwenda Tunduma badala ya pande zote mbili.
Maofisa
hao walimweleza kuwa kuharibika kwa upande huo wa barabara, kunatokana
na malori kutoka Mbeya kwenda Tunduma, kutopimwa uzito kwakuwa hakuna
mizani nyingine kabla ya kufika kituoni hapo.
Hata
hivyo, majibu ya maofisa hayo hayakumridhisha waziri huyo na ndipo
akatupia lawama utendaji kazi wa maofisa wa vituo vya mizani, akisema
umekithiri kwa kupokea rushwa.
Alisema
licha ya serikali kuwafukuza kazi watumishi 400 wa idara hiyo mwaka
jana na kuajiri upya, bado tatizo la upokeaji rushwa kwa watumishi
waliopo ni kubwa mno.
“Mwaka
jana tuliamua kuwafukuza kazi watumishi 400 waliokuwepo kwa kuwa
tuliona wamejikita katika rushwa badala ya kutimiza majukumu yao. Hapo
tukaajiri watu walio na elimu nzuri tukijua tumetibu tatizo. Lakini bado
rushwa inaendelea. Matokeo yake barabara zetu zinaendelea kuharibika,”
alisema.
“Watumishi
wa vituo vya mizani ni mabilionea wakubwa. Hii yote ni kwa kuwa
wanapokea rushwa kutoka kwa watu wanaosafirisha mizigo iliyozidi uzito
na kuharibu barabara zetu,” alisisitiza.
Alisema
ni wakati sasa kwa vyombo vya dola, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na Idara ya Upelelezi ndani ya
Jeshi la Polisi, kufanya uchunguzi kwa maofisa wa vituo vya mizani
nchini.
Alisema
iwapo vyombo hivyo vitalifanyia kazi suala hilo, visisite kuchukua
hatua stahiki kwa watumishi watakaobainika na kuzitaka pia ofisi za
makatibu tawala wa mikoa, kufuatilia suala hilo
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment